Mkutano wa mazingira wa Umoja wa Mataifa waanza Nairobi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i37161-mkutano_wa_mazingira_wa_umoja_wa_mataifa_waanza_nairobi
Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Miroslav Lajčák aliyeko ziarani nchini Kenya, amesema maendeleo hayapaswi kusababisha uharibifu wa mazingira.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 04, 2017 07:11 UTC
  • Mkutano wa mazingira wa Umoja wa Mataifa waanza Nairobi

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Miroslav Lajčák aliyeko ziarani nchini Kenya, amesema maendeleo hayapaswi kusababisha uharibifu wa mazingira.

Aliyasema hayo Jumapili jijini Nairobi, wakati akifunga mjadala kuhusu sayansi, sera na biashara, mjadala uliofanyika kwa siku mbili.

Lajčák amesema hayo akizingatia kuwa harakati za sasa za maendeleo duniani zimekumbwa na vikwazo kama vile majanga ya asili na yale yanayosabishwa na binadamu ambavyo vyote vinatishia siyo tu uwepo wa binadamu bali pia sayari ya dunia.

Hata hivyo amesema tayari sayansi ilitabiri uharibifu wa mazingira, huku nao ujuzi wa asili ukionya dhidi ya  harakati za kupuuza mazingira.

Kwa mantiki hiyo amependekeza mambo matatu, mosi sera zinazotungwa na serikali zitokane na taarifa za kisayansi. Pili ametaka uzingatiaji wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs na mkataba wa mabadiliko ya tabianchi wa Paris akisema nyaraka hizo zitakuwa  hazina maana kama zitapuuzwa.

Miroslav Lajčák akipanda mti mjini Nairobi

Pendekezo la tatu la Bwana Lajčák  ni kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika kuweka mizania ya sera, sayansi na biashara. Hivyo amesema vijana na wadau wengine washirikishwe ili kila mtu atekeleze wajibu huo.

Mapema Bwana Lajčák alishiriki katika tukio la kando kuhusu umuhimu wa misitu ambapo alisema kuwa rasilimali hiyo ni muhimu na pia chanzo muhimu cha uhai.

Alibainisha furaha yake kwa kuweza kushiriki kupanda mti katika msitu wa Karura ulioko mjini Nairobi.

Amekumbusha kuwa misitu ina kazi kubwa pia ya kufyonza hewa ya ukaa ambayo ni  moja ya vyanzo vya mabadiliko ya tabianchi.

Mawaziri wa mazingira kutoka nchi zaidi ya 100 na wajumbe wengine karibu 2,500 wanahudhuria mkutano huo wa mazingira unaonfayika katika makao makuu ya Shirika la Umoja wa Matiafa la Mazingira, UNEP katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.