Uchunguzi wa maoni: Asilimia 85 ya Waganda 'hawamtaki' Museveni
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i37417-uchunguzi_wa_maoni_asilimia_85_ya_waganda_'hawamtaki'_museveni
Uchunguzi wa maoni umeonyesha kuwa asilimia 85 ya wananchi wa Uganda hawaungi mkono muswada wa kufanyia marekebisho katiba ili kuondoa kikomo cha umri wa kugombea urais.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Dec 10, 2017 03:44 UTC
  • Uchunguzi wa maoni: Asilimia 85 ya Waganda 'hawamtaki' Museveni

Uchunguzi wa maoni umeonyesha kuwa asilimia 85 ya wananchi wa Uganda hawaungi mkono muswada wa kufanyia marekebisho katiba ili kuondoa kikomo cha umri wa kugombea urais.

Uchunguzi huo uliofadhiliwa na asasi zisizo za serikali za Citizens Coalition on Electoral Democracy (CEEDU) na Uganda Governance Monitoring Platform (UGMP) umewashirikisha watu zaidi ya 50 elfu kutoka maeneobunge 80 nchini kote, kati ya mwezi Septemba na Novemba.

Dakta Livingstone Sewanyana, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Foundation for Human Rights Initiative amesema utafiti huo umeweka wazi kuwa wananchi wa Uganda wanahisi kadhia hiyo ya kuifanyia katiba marekebisho sio dharura na muhimu kwao, na kwamba kile wangetaka kuona kikishughulikiwa kwa sasa ni masuala ya msingi kama ukosefu wa ajira, malipo duni kwa wafanyakazi wa serikali na kudodora kwa uchumi wa nchi.

Wabunge wa Uganda wakisukumiana makonde wakati wa kujadiliwa muswada huo

Muswada huo wa kuondoa kipengee cha umri wa kugombea urais uliwasilishwa katika bunge la Uganda mwezi Septemba mwaka huu, na kukabiliwa na upinzani mkali kutoka kambi ya wabunge wa upinzani na baadhi ya wale wa chama tawala.

Rais Yoweri Museveni mwenye umri wa miaka 73, ambaye amekuwa madarakani kwa zaidi ya miongo mitatu, kisheria hafai kuwania tena urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2021 kwa sababu katiba ya Uganda imeainisha miaka 75 kuwa kikomo cha umri wa mtu anayetaka kugombea urais.