Libya na Italia zakubaliana kuanzisha oparesheni za kukabiliana na magendo ya wahajiri
Serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa imekubaliana na Italia kuanzisha vyumba vya pamoja vya oparesheni ili kukabiliana na magendo ya wahajiri kama sehemu ya juhudi za kukomesha wimbi la wahajiri kuelekea Ulaya.
Itafahamika kuwa, Libya ni lango kuu linalotumiwa na wahamiaji haramu wanaojaribu kuelekea Ulaya kwa kutumia njia ya bahari japokuwa idadi yao imepungua kwa kiasi kikubwa tangu mwezi Julai mwaka huu tangu makundi na maafisa husika wa Libya waanze kuzuia safari za wahamiaji kuelekea katika nchi za Ulaya kufuatia mashinikizo ya Italia.

Makubaliano hayo ya kuanzisha vyumba vya pamoja vya oparesheni yalifikiwa baada ya kufanyika mkutano huko Tripoli baina ya Fayyez al Seraj Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya, Aref Khodja Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo na mwenzake wa Italia, Marco Minniti.
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Libya imeeleza kuwa vituo hivyo vitakuwa na wawakilishi kutoka kitengo cha ulinzi wa maeneo ya pwani, mwanasheria mkuu wa Libya, idara za kiitelijinsia pamoja na wenzao wa Italia.