Amnesty yasema EU inashiriki katika kuteswa wahajiri Libya
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limezituhumu nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kuwa zinashiriki katika kuteswa, kukandamizwa na kudhalilishwa wahajiri wanaozuiliwa nchini Libya.
Katika ripoti yake iliyoitoa leo Jumanne, Amnesty imesema EU imekuwa ikifumbia macho jinai wanazofanyiwa wahamiaji na maafisa wa Gadi ya Pwani ya Libyahao katika jela za kutisha .
John Dalhuisen, Mkurugenzi wa Amnesty International barani Ulaya amesema, na hapa tunanukuu: "Nchi za Ulaya sio tu zinafahamu fika kuhusu jinai hizo, bali ni 'mshiriki' wa moja kwa moja. Tuna kanda za video zinazoonyesha namna boti ya Italia ilivyotumika katika operesheni ya kuwakamata wahajiri, ambapo 50 miongoni mwao walikufa maji."
Ripoti ya Amnesty International imebainisha kuwa, hatua ya EU ya kuwapa mafunzo na silaha wanajeshi wa Gadi ya Pwani ya Libya kwa ajili ya kukabiliana na wahajiri wanaotaka kwenda barani Ulaya, imepelekea kukamatwa kwa wahamiaji zaidi ya 20 elfu, ambao kwa wanazuiliwa katika mazingira ya kuogofya.
Hii ni katika hali ambayo, Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Ghassan Salamé amesema kuwa, ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Libya umefikia kiwango cha kutia wasiwasi.
Itafahamika kuwa, Libya sio tu kitovu cha biashara haramu ya utumwa, bali pia ni lango kuu linalotumiwa na wahamiaji haramu wanaojaribu kuelekea Ulaya kwa kutumia njia ya bahari.