Watu 170 wauawa katika mapigano ya kikabila Sudan Kusini
Watu zaidi ya 170 wamethibitishwa kuuawa Sudan Kusini katika mapigano ya kikabila yaliyoibuka katika eneo la Maziwa Makuu nchini humo wiki iliyopita.
Akizungumza na waandishi habari Jumanne hii, mbunge kutoka eneo hilo Dharua Mabor Teny amesema idadi hiyo imepanda kutoka 45 hadi 170 na kuongeza kuwa watu wengine 1,800 wameachwa bila makazi na nyumba 342 kuteketezwa moto.
Mapigano katika Kaunti ya Malek yaliibuka wakati vijana kutoka kabila la Ruop walipowashambulia vijana kutoka kabila la Pakam Jumatano na Alhamisi wiki jana. Aidha amesema mashambulizi ya kulipiza kisasi yamejiri tokea mapigano ya awali.
Mapigano hayo yalipelekea serikali kutangaza hali ya hatari kwa muda ya miezi mitatu katika eneo hilo siku ya Jumatatu. Aidha jeshi limetuma askari wake katika eneo hilo kujaribu kutuliza hali ya mambo.
Shadrack Bol Maachok, msemaji wa serikali katika eneo hilo, amesema kuwepo idadi kubwa ya silaha mikononi mwa wananchi ni jambo ambalo limefanya iwe vigumu kudhibiti uhasama.
Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Nchi hiyo, ambayo ilijitenga na Sudan mwaka 2011, ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake.