Dec 14, 2017 07:42 UTC
  • Watu watano wauawa na wanamgambo wa Boko Haram Nigeria

Watu wasiopungua watano wameuawa katika shambulio la hivi kkaribuni kabisa la wanamgambo wa Boko Haram nchini Nigeria kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, wanachama wa kundi la Boko Haram alasiri ya jana waliwatia mbaroni watu watano waliokuwa wakikimbia kutoka katika eneo la Damboa lililoko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo na kuwaua kinyama.

Babakura Kolo mkuu wa kundi moja la wanamgambo linalopigana bega kwa bega na jeshi la Nigeria dhidi ya wanamgambo wa Boko Haram amesema kuwa, watu hao walikuwa wakikimbia mashambulio ya Boko Haram katika kijiji hicho.

Baadhi ya ripoti zinaeleza kuwa, kwa sasa wanamgambo wa Boko Haram wameshadidisha harakati zao katika eneo la Damboa na wamekuwa wakiwashambulia na kuwaua kiholela raia na hata wale wanaotaka kukimbia na kulihama eneo hilo.

Rais Muhamadu Buhari wa Nigeria

Mashambulizi ya genge la kigaidi la Boko Haram yalianza mwaka 2009 kaskazini na kaskazini mashariki mwa Nigeria na hadi hivi sasa zaidi ya watu 20 elfu wameshauawa kutokana na hujuma na machafuko  yaliyosababishwa na kundi hilo.

Kundi la Boko Haram limekuwa likifanya jinai za kila namna ikiwa ni pamoja na kuteka nyara watu pamoja na wasichana na kuwapiga mnada kama bidhaa. 

Serikali ya Rais Muhamadu Buhari imeendelea kukosolewa kutokana na kushindwa kukabiliana na kundi hilo ambalo kwa sasa limepanua harakati zake hadi katika nchi jirani za Cameron, Niger na hata Chad.

Tags