EU: Tumeandaa mpango maalumu wa kuwaondoa wahajiri 15 elfu nchini Libya
Mkuu wa Siasa za Kigeni za Umoja wa Ulaya amesema kuwa umoja huo umeandaa mpango maalumu wa kuwaondoa wahajiri 15 wa Kiafrika kutoka katika ardhi ya Libya.
Federica Mogherini alisema hayo jana mjini Brussels, Ubelgiji, na kuongeza kuwa, Umoja wa Ulaya una matumaini kwamba utaweza kuwarejesha makwao kwa hiari wahajiri 15 elfu wa Kiafrika hadi mwezi Februari 2018.
Amesema, kiujumla ni kwamba tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi hivi sasa, wahajiri waliofaidika na msaada wa kurejeshwa nyumbani kwa hiari kutoka nchini Libya wamefikia watu 30 elfu.
Hivi sasa kuna timu maalumu ambayo imepewa jukumu la kufanya kazi hiyo. Timu inaundwa na Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya, Shirika la Kimataifa la Wahajiri pamoja na Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR.
Timu hiyo iliundwa kwenye kikao cha Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya kilichofanyika mjini Abidjan, Ivory Coast mwishoni mwa mwezi uliopita wa Novemba na ndiyo ambayo hivi sasa inapanga mikakati ya kuwarejesha makwao wahajiri wa Kiafrika waliokwama nchini Libya.
Hatua hizo zimechukuliwa baada ya jamii ya kimataifa kukasirishwa sana na picha na mikanda ya video iliyoonesha namna wahajiri wa Kiafrika wanavyopigwa mnada na kuuzwa kama bidhaa katika masoko ya watumwa nchini Libya.