Rais wa Zimbabwe ameazimia kupambana na ufisadi
Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe ameazimia kupambana na ufisadi na kusema atawataja na kuwaaibisha wote waliopeleka fedha za umma nje ya nchi kama watashindwa kuzirudisha.
Rais Mnangagwa alitoa muda wa miezi mitatu itakayomalizika mwishoni mwa mwezi Februari mwakani kwa wote waliopeleka pesa za umma nje ya nchi kuzirudisha bila kuulizwa wala kukamatwa. Amesema kuwa tayari ana orodha ya majina yao, na wasipofanya hivyo atawafedhehesha.
Ikiwa ni moja ya hatua ya kufufua uchumi, Rais Mnangagwa pia amesema, umefika wakati kwa chama tawala kubadilisha mwelekeo, na kuangalia uchumi na sio siasa peke yake.
Mbali na kuchukua hatua ndani ya nchi, Rais Mnangagwa ametoa mwito kwa nchi za Magharibi kuondoa vikwazo dhidi ya Zimbabwe. Kauli hiyo imekuja wakati Marekani ikiwa imesema itaendelea na vikwazo dhidi ya Zimbabwe hadi nchi hiyo itakapoahidi kutekeleza mageuzi ya kisiasa.
Mnangagwa aliapishwa kuwa rais mpya wa Zimbabwe tarehe 24 Novemba, yaani siku tatu baada ya rais wa zamani wa nchi hiyo, Robert Mugabe kulazimishwa kujiuzulu.