WHO: Mamia wamefariki dunia Sudan Kusini kutokana na kipindupindu
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa, watu 462 wamefariki dunia nchini Sudan Kusini tangu ugonjwa wa kipindupindu ulipotangazwa nchini humo mwezi Juni mwaka jana na kwamba wengine 21 elfu na 571 wanasumbuliwa na maradhi hayo.
Taarifa ya WHO iliyotolewa jana Ijumaa imesema kuwa, hilo ni wimbi kubwa zaidi na la muda mrefu la maambukizi ya kipindupindu nchini Sudan Kusini ambalo linazidisha migogoro kama ya ukosefu wa amani, wakimbizi na uhaba wa maji salama ya kunywa.
Shirika la Afya Duniani limeongeza kuwa, kuna matumaini kwamba serikali ya Sudan Kusini itafanikiwa kupunguza idadi ya vifo vya watu kutokana na kipindupindu kwa kutumia misaada ya shirika hilo na kutoa chanjo inayohitajika.
Sudan Kusini ilitumbukia katika mapigano ya ndani mwaka 2013 baada ya Rais Salva Kiir wa nchi hiyo kumtuhumu aliyekuwa makamu wake, Riek Machar kwamba alifanya jaribio la kupindua serikali yake.