Matumaini Sudan Kusini baada ya Machar kuamuru wafuasi wake wasitishe vita
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i37997-matumaini_sudan_kusini_baada_ya_machar_kuamuru_wafuasi_wake_wasitishe_vita
Matumaini ya amani Sudan Kusini yameimarika baada ya kiongozi wa waasi, Riek Machar kuamuru wapiganaji wake kuacha kupigana na wanajeshi wa serikali.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 23, 2017 23:56 UTC
  • Matumaini Sudan Kusini baada ya Machar kuamuru wafuasi wake wasitishe vita

Matumaini ya amani Sudan Kusini yameimarika baada ya kiongozi wa waasi, Riek Machar kuamuru wapiganaji wake kuacha kupigana na wanajeshi wa serikali.

Hatua hii imekuja baada ya pande mbili zinazozana kutia saini mkataba wa kusitisha mapigano siku ya Alhamisi jijini Addis Ababa nchini Ethiopia, kufuatia mazungumzo ya amani yaliyoongozwa na Jumuiya ya Kieneo ya Kiserikali ya Maendeleo ya Nchi za Mashariki mwa Afrika (IGAD).

 Mapatano hayo yanalenga kuhuisha makubaliano ya amani ya mwaka 2015 ambayo yalivunjika mwaka jana baada ya kuibuka mapigano katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba.

Salva Kiir na Riek Machar

Hata hivyo Machar ambaye anaishi uhamishoni nchini Afrika Kusini, amewaambia wapiganaji wake wajilinde iwapo watashambuliwa.

Hakujawa na uhakika iwapo mkataba huo utaheshimiwa kwa sababu siku ya Ijumaa, makabiliano mapya kati ya waasi na wanajeshi wa serikali yalizuka katika majimbo ya Bahr el Ghazal, Upper Nile na Equatorial.

Sudan Kusini ilitumbukia katika vita vya ndani Disemba 2013 baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kuipindua serikali yake.