Kuanza kutekelezwa usitishaji vita nchini Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i38015-kuanza_kutekelezwa_usitishaji_vita_nchini_sudan_kusini
Utekelezaji wa usitishaji vita huko Sudan Kusini umeanza kutekelezwa kwa shabaha ya kuhitimisha vita vya ndani katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika kufuatia makubaliano yaliyofikiwa kati ya pande zinazozozana katika nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 24, 2017 10:11 UTC
  • Kuanza kutekelezwa usitishaji vita nchini Sudan Kusini

Utekelezaji wa usitishaji vita huko Sudan Kusini umeanza kutekelezwa kwa shabaha ya kuhitimisha vita vya ndani katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika kufuatia makubaliano yaliyofikiwa kati ya pande zinazozozana katika nchi hiyo.

Baada ya miaka minne ya vita vilivyokuwa na uharibifu mkubwa baina ya waasi na serikali ya Sudan Kusini, hatimaye serikali ya Juba hivi karibuni ilitiliana saini makubaliano ya kuacha uhasama na makundi muhimu ya waasi na kwa mujibu wa makubaliano hayo, usitishaji vita umeanza kutekelezwa. Makubaliano hayo yalitiwa saini huko Addis Ababa Ethiopia yalipo makao makuu wa Umoja wa Afrika kati ya Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na wapinzani kwa uongozi wa Riek Machar makamu wake wa zamani kwa usimamizi wa Jumuiya ya Kieneo ya IGAD.

Kupitia makubaliano hayo, pande husika zimekubaliana kusitisha vita kuanzia leo tarehe 24 Desemba, kulindwa raia na kuruhusiwa misaada ya kibinadamuu kuwafikia.

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini

Makubaliano ya usitishaji vita yametiwa saini katika hali ambayo, kwa miaka kadhaa sasa Sudan Kusini imekuwa uwanja wa vita na mapigano kati ya waungaji mkono wa Rais Salva Kiir na wapinzani wake wanaoongozwa na Riek Machar. Machafuko hayo yamepelekea maelfu ya watu kuuawa, kujeruhiwa na wengine wengi kuwa wakimbizi. Makubaliano ya usitishaji vita Sudan Kusini yamepokelewa kwa mikono miwili kieneo na kimataifa.

Moussa Faki Mahamat, Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amesema kuwa: Umoja huo unaunga mkono makubaliano ya amani yaliyofikiwa kati ya serikali ya Sudan Kusini na makundi ya waasi katika nchi hiyo na unaamini kwamba, makubaliano hayo ni hatua ya kwanza madhubuti kwa ajili ya kuhitimisha mapigano na mauaji huko Sudan Kusini yaliyoanza Disemba mwaka 2013.

Kutiwa saini hati ya makubaliano ya usitishaji vita kumefanyika katika hali ambayo, kuendelea mapigano hayo kumesababisha kuibuka mgogoro mkubwa wa kibinadamu katika nchi hiyo. Mark Lukok, Naibu Katibu Mkuuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya kibinadamu ametangaza katika ripoti yake kwamba, zaidi ya watu milioni moja na laki mbili huko Sudan Kusini wanajongewa na hatari ya ukame na baa la njaa.

Wakimbizi wa Sudan Kusini

Hali hiyo haiikabili Sudan Kusini tu, bali nchi zinazopakana nayo nazo zina hali hiyohiyo kutokana na kukabiliwa na ongezeko la wakimbizi. Karibu raia milioni mbili wameyakimbia makazi yao huko Sudan Kusini na kukimbilia katika maeneo salama ndani ya nchi hiyo huku wengine milioni mbili wakikimbilia katika nchi jirani wakihofia usalama wa maisha yao. Hali hiyo imepelekea kutokea moja ya migogoro mibaya kabisa ya wakimbizi katika uga wa kimataifa.

Wajuzi wengi wa mambo wanaamini kuwa, chimbuko la mgogoro wa Sudan Kusini ni hitilafu na mizozo ya kikaumu na kikabila, kutokuweko miundo mbinu ya lazima na kukosekana utayari wa kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa ajili ya nchi hiyo kujitenda na Sudan, na kubwa kuliko yote ni kuweko mivutano ya nyuma ya pazia ya baadhi ya madola ya kuwa na uwepo katika nyuga mbalimbali katika nchi hiyo hasa kwa kuzingatia maliasi na utajiri ulioko katika nchi hiyo pamoja na nafasi yake.

Hii ni mara ya pili kufikiwa makubaliano ya kuhitimisha mgogoro na vita huko Sudan Kusini baina ya pande mbili hasimu. Licha ya kuwa makubaliano yaliyotiwa saini miaka kadhaa iliyopita nayo yalileta matumaini ya kuhitimishwa mgogoro wa kisiasa katika nchi hiyo, lakini hivi sasa mgogoro wa Sudan Kusini umekuwa mkubwa zaidi ikilinganishwa na huko nyuma.