Umoja wa Mataifa wataka kufanyika uchaguzi Libya mwaka huu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i38799-umoja_wa_mataifa_wataka_kufanyika_uchaguzi_libya_mwaka_huu
Umoja wa Mataifa umesema uko tayari kuisaidia Libya katika maandalizi ya uchaguzi mkuu kufikia mwishoni mwa mwaka huu 2018.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 11, 2018 00:29 UTC
  • Umoja wa Mataifa wataka kufanyika uchaguzi Libya mwaka huu

Umoja wa Mataifa umesema uko tayari kuisaidia Libya katika maandalizi ya uchaguzi mkuu kufikia mwishoni mwa mwaka huu 2018.

Jeffrey Feltman, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Siasa amesema kufanyika uchaguzi mwaka huu ni hatua muhimu ya kuelekea katika amani ya kudumu na kutamatisha kipindi cha mpito kwa kuzijumuisha pande zote hasimu za kisiasa.

Hivi sasa kuna serikali mbili zinazoshikilia hatamu za madaraka nchini Libya. Moja ni serikali ya umoja wa kitaifa inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ambayo iko kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli inayoongozwa na Fayez Siraj, na nyengine ni serikali iliyoko mashariki mwa nchi ambayo inaungwa mkono na Bunge na baadhi ya vikosi vya ulinzi vinavyoongozwa na Khalifa Haftar.

Feltman amesema Umoja wa Mataifa umetiwa moyo sana na hamasa ya wananchi kujitokeza kwa wingi kusajiliwa kuwa wapiga kura.

Fayez Siraj na Khalifa Haftar 'wakipatanishwa' na Rais wa Ufaransa

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi nchini humo, zaidi ya watu laki tano wamesajiliwa kuwa wapiga kura wapya tangu shughuli ya usajili ianze mapema mwezi uliopita wa Disemba.

Kwa sasa kuna zaidi ya wapiga kura milioni 1 na laki 9, katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika yenye watu zaidi ya milioni 6.

Katika uchaguzi wa mwaka 2014, wapiga kura 630,000 tu ndio waliojitokeza kutekeleza wajibu wao huo wa kidemokrasia.