Jan 11, 2018 15:56 UTC
  • Watu kadhaa wauawa katika shambulio jipya la Boko Haram nchini Cameroon

Duru za kiusalama nchini Cameroon zimetangaza habari ya kutokea shambulizi jipya la genge la kigaidi la Boko Haram kaskazini mwa nchi hiyo.

Duru hizo zimesema leo (Alkhamisi) kwamba watu watatu wameuawa baada ya magaidi wa Boko Haram kufanya shambulio katika eneo la Kolofata, kaskazini mwa Cameroon, karibu na mpaka wa nchi hiyo na Nigeria.

Duru hizo zimeongeza kuwa, shambulio hilo lilitokea jana usiku wakati magaidi hao walipolivamia eneo hilo kwa ajili ya kupora chakula.

Raia wa kawaida, wanawake na watoto wadogo, wahanga wakuu wa jinai za Boko Haram

 

Duru za usalama za Cameroon zimesisitiza pia kuwa, kundi la wakufusiahji la Boko Haram Jumatano usiku lilivamia vijiji kadhaa katika eneo la Mayo-Moskota, kaskazini mwa Cameroon na kufanya uhalifu mkubwa.

Genge la Boko Haram lilizuka mwaka 2009 nchini Nigeria kwa madai ya kupambana na elimu zinazotoka nchi za Magharibi. Tangu wakati huo hadi hivi sasa Nigeria inaendelea kushuhudia mashambulizi ya mara kwa mara ya magaidi hao hususan eneo la kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. 

Mwaka 2015 magaidi wa Boko Haram walipanua wigo wa mashambulio yao hadi katika nchi jirani za Niger, Chad na Cameroon.

Hadi hivi sasa zaidi ya watu 20 elfu wameshauawa katika nchi hizo nne za Nigeria, Cameroon, Niger na Chad kutokana na mashambulizi ya Boko Haram na zaidi ya milioni mbili wengine wamekuwa wakimbizi.

Tags