Jeshi la Kongo lazindua operesheni dhidi ya waasi wa ADF wa Uganda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i38947-jeshi_la_kongo_lazindua_operesheni_dhidi_ya_waasi_wa_adf_wa_uganda
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limeanzisha operesheni kali dhidi ya kundi la ADF la Uganda katika mji wa Beni mashariki mwa nchi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 14, 2018 04:19 UTC
  • Jeshi la Kongo lazindua operesheni dhidi ya waasi wa ADF wa Uganda

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limeanzisha operesheni kali dhidi ya kundi la ADF la Uganda katika mji wa Beni mashariki mwa nchi.

Jenerali Marcel Mbangu, kamanda mkuu wa jeshi la Kongo katika mkoa wa Kivu Kaskazini amesema operesheni hiyo dhidi ya maficho ya waasi hao na iliyoanza jana Jumamosi ni sehemu ya jitihada za pamoja za jeshi la nchi hiyo na lile la Uganda, za kulitokomeza kundi hilo la waasi.

Amesema: "Hii ni operesheni yetu ya mwisho, tutapmbana kufa kupona hadi tuhakikishe tumelinda mipaka yetu."

Uganda na Kongo DR zilikubaliana kuimarisha utaratibu wa mawasiliano na kupeana taarifa za kiintelijensia kwa ajili ya kupambana na waasi hao wanaotokea Uganda ambao wanaendesha harakati zao mashariki mwa DRC, baada ya askari 14 wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)  na watano wa DRC kuuawa mwanzoni mwa mwezi uliopita wa Disemba, katika kambi ya Semuliki mkoani Kivu Kaskazini kufuatia hujuma ya waasi hao wa ADF.

Askari wa Kongo DR wakimkamata mmoja wa waasi wa ADF

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Jeshi la Uganda lilitangaza habari ya kuua wanachama wasiopungua 100 wa kundi la waasi wa ADF katika makabiliano makali yaliyojiri mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Wanajeshi wa Tanzania na Kongo waliouawa mapema mwezi jana walikuwa ni sehemu ya askari 3,000 wa timu ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa MONUSCO yenye askari kutoka Tanzania, Malawi na Afrika Kusini.