Mwandishi habari wa Marekani apigwa na waandamanaji Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i40015-mwandishi_habari_wa_marekani_apigwa_na_waandamanaji_sudan_kusini
Wananchi waliokuwa na hasira Jumanne walimpiga vibaya mwandishi habari wa Marekani katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba wakati wa maandamano ya kupinga vikwazo vya silaha vya Marekani dhidi ya nchi hiyo.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Feb 06, 2018 23:05 UTC
  • Mwandishi habari wa Marekani apigwa na waandamanaji Sudan Kusini

Wananchi waliokuwa na hasira Jumanne walimpiga vibaya mwandishi habari wa Marekani katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba wakati wa maandamano ya kupinga vikwazo vya silaha vya Marekani dhidi ya nchi hiyo.

Maandamano hayo yaliandaliwa na makundi kadhaa ya vijana ikiwemo Jumuiya ya Vijana ya chama tawala SPLM.

Tukio hilo lilijiri katika kambi ya Umoja wa Mataifa karibu na Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Juba. Walioshuhudiwa tukio hilo wanasema waandamanaji walionekana kuchukizwa na waandishi habari wa kigeni hasa Wamarekani.

Siku ya Ijumaa, Marekani ilitangaza kuiwekea vikwzo vya silaha Sudan Kusini kwa madai kuwa vita vya ndani vinavyoendelea katika nchi hiyo havionekani kuwa na matumaini ya kumalizika.

Salva Kiir na Riek Machar

Wakati huo huo Jumuiya ya Maendeleo ya Serikali ya Nchi za Afrika Mashariki IGAD imeanzisha tena mazungumzo ya amani kuhusu Sudan Kusini huko Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, ambayo imetishia kuchukua hatua za kuziadhibu pande mbalimbali zinazopigana.

Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Nchi hiyo ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake.