Harakati Ya Kiislamu Nigeria yataka haki itendeke kuhusu wafuasi wake waliouawa
Wafuasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria wameandamana kwa mnasaba wa Siku ya Arubaini ya kuuawa wafuasi kadhaa wa harakati hiyo wakati wakishiriki katika maandamano ya kutaka Sheikh Ibrahim Zakzaky aachiliwe huru.
Wafuasi wa harakati hiyo mwaka huu wameanzisha kampeni mpya ya maandamano kaskazini mwa nchi hiyo na mji mkuu Abuja wakitaka serikali imuachilie huru mwanazuoni huyo. Badala ya serikali kutii amri ya mahakama ya kumuachilia huru, maafisawa polisi waliwafyatulia risasi na kuwaua wafuasi kadhaa wa harakati hiyo katika miji ya Abuja, Kaduna na Zaria.
Itakumbukwa kuwa, Sheikh Ibrahim Zakzaky alitiwa nguvuni na jeshi la Nigeria mwezi Disemba mwaka 2015 baada ya kuvamia makazi yake katika mji wa Zaria jimboni Kaduna na kufanya mauaji ya umati dhidi ya Waislamu. Taarifa zinasema mamia ya Waislamu waliuawa shahidi katika hujuma hiyo wakiwemo watoto watatu wa Sheikh Zakzaky.
Hata hivyo licha ya mahakama kutoa hukumu ya kutaka kuachiwa huru mwanazuoni huyo, bado vyombo vya usalama vya Nigeria vinaendelea kumshikilia katika korokoro isiyojulikana huku ripoti zikifichua kwamba hali yake ya kiafya ni mbaya.