CCM yatwaa majimbo ya Kinondoni na Siha, askari 6 wakamatwa mauaji ya mwanachuo
Chama cha Mapinduzi (CCM) huko nchini Tanzania kimetangazwa mshindi wa chaguzi ndogo za majimbo ya Siha mkoani Kilimanjaro na Kinondoni jijini Dar es Salaam ambayo kabla ya kujiuzulu wabunge wake yalikuwa mikononi mwa vyama vya upinzani.
Kwa mujibu wa Tume Taifa ya Uchaguzi NEC, Godwin Oloyce Mollel wa Chama cha Mapinduzi amepata ushindi kwa kupata kura 25,611 katika jimbo la Siha huku mpinzani wake, Elvis Mosi wa Chadema akipata kura 5,905.
Kwa upande wa Kinondoni, tume hiyo imemtangaza Said Mtulia kuwa mshindi kwa kura 30,247, akifuatiwa na Salum Mwalimu wa Chadema aliyepata 12,353, Rajab Salum wa CUF (1,943) na Ally Abdallah wa ADA-TAPEA (97).
Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Chadema ilishinda katika Jimbo la Siha kupitia Dkt Godwin Mollel huku CUF ikilitwaa jimbo la Kinondoni kupitia kwa Maulid Said Mtulia.
Wabunge hao walihama upinzani kwa kile walichodai kuwa wanaunga mkono juhudi za serikali iliyopo madarakani, jambo ambalo liliifanya Tume ya Uchaguzi (Nec) kuitisha uchaguzi mdogo katika majimbo hayo mawili.
Huku hayo yakiarifiwa, jeshi la polisi nchini Tanzania linawashikilia askari wake sita kwa ajili ya uchunguzi wa tukio la kuuawa kwa risasi mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji NIT anayejulikana kwa jina Aquillina Akwilini, mbali na watuhumiwa wengine 40.
Aidha serikali ya Tanzania kupitia Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako imesema itagharamia mazishi ya mwanachuo huyo.
Vincent Mashinji, Katibu Mkuu wa Chadema anasisitiza kuwa polisi ndio waliomuua mwanafunzi huyo kwa kumfyatulia risasi.