Sudan Kusini yakaribia kukumbwa na baa jingine la njaa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i40907-sudan_kusini_yakaribia_kukumbwa_na_baa_jingine_la_njaa
Karibu theluthi mbili ya jamii nzima ya watu wa Sudan Kusini wanahitaji misaada ya chakula ili kukabiliana na njaa. Hayo yameelezwa na maafisa wa serikali na Umoja wa Mataifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 26, 2018 11:05 UTC
  • Sudan Kusini yakaribia kukumbwa na baa jingine la njaa

Karibu theluthi mbili ya jamii nzima ya watu wa Sudan Kusini wanahitaji misaada ya chakula ili kukabiliana na njaa. Hayo yameelezwa na maafisa wa serikali na Umoja wa Mataifa.

Maafisa wa misaada ya kibinadamu wamesema leo kuwa Sudan Kusini inakaribia kukumbwa na njaa baada ya kupita zaidi ya miaka minne ya vita vya wenyewe kwa wenyewe na makubaliano kadhaa ya kusimamisha vita yaliyogonga mwamba. Wajumbe wa jopokazi linalowajumuisha maafisa wa Sudan Kusini na wa Umoja wa Mataifa wameeleza kuwa karibu theluthi mbili ya raia wa nchi hiyo watahitajia misaada ya chakula mwaka huu ili kukabiliana na tatizo la njaa na utapiamlo.

Utapiamlo miongoni mwa raia wa Sudan Kusini khususan watoto wadogo kutokana na baa la njaa  

Serge Tissot Afisa wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) huko Sudan Kusini amesema kuwa hali ya mambo ni ya kulegalega kikamilifu na kwamba nchi hiyo inakaribia kuathiriwa na baa jingine la njaa. Utafiti uliofanywa na jopokazi hilo umeonyesha kuwa, jumla ya watu milioni 5.3 sawa na asilimia 48 ya jamii ya Sudan Kusini hivi sasa wako katika hali ya mgogoro au kwa maneno mengine hali ya dharura. Amesema inaonekana kuwa mwaka huu utakuwa mwaka mgumu zaidi kwa raia wa Sudan Kusini.