Mali inachunguza tuhuma kuwa askari wake wameuwa raia
Serikali ya Mali imesema kuwa inachunguza tuhuma zilizotolewa na chama cha upinzani nchini humo kuwa jeshi la nchi hiyo liliwateka nyara na kuwauwa raia saba katikati mwa nchi hiyo wiki iliyopita.
Chama hicho cha upinzani cha SADI kimelituhumu jeshi la Mali kuwa liliwauwa wanaume saba waliokuwa wakishiriki hafla ya kidini katika kijiji cha Nangarabakan katika mkoa wa Segou tarehe 21 mwezi huu. Wahanga hao ni pamoja na imamu na watu kadhaa kutoka familia ya kiongozi wa kijiji.
Serikali ya Mali jana jioni ilitoa taarifa ikithibitisha kuuliwa raia hao. Ilisema watu hao waliuawa katika oparesheni ya kuwasaka wanamgambo wenye silaha katikati mwa nchi hiyo, eneo ambalo limekuwa likikabiliwa na mashambulizi ya wanamgambo wanaobeba silaha. Serikali ya Bamako imesema imeagiza kufanyike uchunguzi kuhusiana na mauaji hayo.
Serikali ya Mali imetuma salamu za rambimbai kwa familia za wahanga wa mauaji hayo na kukariri azma yake ya kusonga mbele na oparesheni ya kuwasaka wanamgambo wenye silaha.