Askari wanne wa Somalia wauawa katika shambulio la bomu karibu na Mogadishu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i41493
Askari wasiopungua wanne wa vikosi vya usalama vya Somalia wameuawa na mwengine mmoja amejeruhiwa katika mripuko wa bomu uliotokea kwenye viunga vya mji mkuu wa nchi hiyo Mogadishu.
(last modified 2025-07-23T09:10:30+00:00 )
Mar 11, 2018 07:18 UTC
  • Askari wanne wa Somalia wauawa katika shambulio la bomu karibu na Mogadishu

Askari wasiopungua wanne wa vikosi vya usalama vya Somalia wameuawa na mwengine mmoja amejeruhiwa katika mripuko wa bomu uliotokea kwenye viunga vya mji mkuu wa nchi hiyo Mogadishu.

Polisi imetangaza kuwa shambulio hilo ambalo lilitokea jana jioni liliwalenga askari hao walipokuwa wakipita kwenye kijiji cha Weydow kilichoko kilomita chache nje ya mji mkuu huo wa Somalia.

Afisa mmoja wa polisi ambaye hakutaka kutajwa jina lake amevieleza vyombo vya habari kuwa: "askari wanne walifariki katika shambulio la bomu walipokuwa wakipita eneo la Weydow".

Wakaazi wa eneo hilo wamesema walisikia sauti ya mripuko iliyofuatiwa na milio ya risasi.

Wanamgambo wa kundi la kigaidi la Ash-Shabab

Fos Ahmed, mkazi wa kijiji cha Weydow amesema: "tulisikia mlio mkubwa kutokea eneo walipokuwa wakipita askari wa Somalia. Niliona pia gari la kubebea wagonjwa linaelekea eneo la tukio".

Japokuwa hadi tunaelekea mitamboni hakuna kundi lililotangaza kuhusika na shambulio hilo la jana, lakini kundi la kigaidi la Ash-Shabab limeshadidisha mashambulio ya aina hiyo dhidi ya vikosi vya serikali ya Somalia katika wiki za karibuni.

Shambulio hilo limejiri huku operesheni za mashambulio dhidi ya kundi hilo la kigaidi zikiwa zinaendelea kusini mwa nchi hiyo.../