Mgombea wa upinzani nchini Sierra Leone aongoza huku duru ya pili ikitarajiwa
Matokeo ya awali ya uchaguzi wa Rais yanayoendelea kutangazwa nchini Sierra Leone yanaonesha kuwa, mgombea wa upinzani anaongoza huku akiwa amemuacha mbali mgombea wa chama tawala kwa zaidi ya kura elfu 15.
Mgombea wa upinzani Julius Maada Bio amepata asilimia 43.5 ya kura dhidi ya asilimia 42.6 alizopata mgombea wa chama tawala Samura Kamara huku tume ya uchaguzi ikiwa imehesabu karibu asilimia 75 ya kura zote.
Muungano wa kitaifa unaoongozwa na mwanadiplomasia wa zamani kwenye Umoja wa Mataifa Kandeh Yumkella ambaye anatarajia kugawa kura za wagombea vinara, yeye amepata asilimia 6.69 ya kura zote.
Matokeo rasmi ya uchaguzi uliofanyika juma lililopita yanatarajiwa kutangazwa ndani ya siku chache zijazo lakini kwa matokeo haya ni wazi kuwa huenda kukawa na duru ya pili ya uchaguzi kwa kuwa hakuna mgombea ambaye huenda akafikisha ushindi wa asilimia 55 unaotakiwa kikatiba.
Zaidi ya Wasierra Leone milioni tatu waliokamilisha masharti walikwenda kwenye masanduku ya kupigia kura kuchagua rais wa nchi na wawakilishi wao katika Bunge la nchi hiyo. Wagombea 16 walichuana kuwania kiti cha rais ingawa ushindani mkubwa zaidi ulikuwa baina ya mgombea wa chama tawala, Samura Kamara na yule wa chama cha Sierra Leone People’s, Julius Maada Bio.
Kwa mujibu wa Katiba ya Sierra Leone, Rais anayemaliza muda wake, Ernest Bai Koroma hawezi kugombea tena kiti hicho kwa mara ya tatu baada ya kuongoza nchi hiyo kwa vipindi viwili.