WFP: Watu milioni 7 wanakabiliwa na njaa Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i41615-wfp_watu_milioni_7_wanakabiliwa_na_njaa_sudan_kusini
Zaidi ya watu milioni saba kati ya milioni 12 nchini Sudan Kusini huenda wakakabiliwa na uhaba wa chakula katika miezi michache ijayo kusipopatikana misaada ya kibinadamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 13, 2018 23:14 UTC
  • WFP: Watu milioni 7 wanakabiliwa na njaa Sudan Kusini

Zaidi ya watu milioni saba kati ya milioni 12 nchini Sudan Kusini huenda wakakabiliwa na uhaba wa chakula katika miezi michache ijayo kusipopatikana misaada ya kibinadamu.

Tahadhari hiyo limetolewa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) ambalo sasa linahaha kupata fedha za kutosha kwa ajili ya kutoa msaada kwa watu hao.

Maelfu ya wakimbizi wa Sudan Kusini wanaendelea kumiminika katika nchi jirani ikiwemo Kenya ambako kambi ya Kakuma inahifadhi zaidi wakimbizi 106,000 kutoka sudan kusini. WFP inawapa msaada wa chakula wanapopokelewa tu. Msemaji wa WFP  nchini Kenya, Martin Karimi anasema wanapokea takribani watu elfu moja kila mwezi. Ameongeza kuwa wanapowasili, WFP inawapa mlo wa moto kabla hawajapewa makazi ambako wataendelea kupokea mgao wa chakula pamoja na fedha taslimu kutoka WFP.

Salva Kiir (kushoto) na Riek Machar

Hivi sasa WFP inatoa wito kwa wahisani na wafadhili kutoa fedha ili kusaidia shirika hilo kuokoa maisha ya maelfu ya wakimbizi hao.

Sudan Kusini ilitumbukia katika vita vya ndani Disemba 2013 baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kuipindua serikali yake.