Algeria imewarejesha nyumbani wahajiri elfu 27 wa Kiafrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i42052-algeria_imewarejesha_nyumbani_wahajiri_elfu_27_wa_kiafrika
Serikali ya Algeria imewarejesha katika nchi zao makumi ya maelfu ya wahajiri wa Kiafrika waliokuwa wamemiminika katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 23, 2018 02:49 UTC
  • Algeria imewarejesha nyumbani wahajiri elfu 27 wa Kiafrika

Serikali ya Algeria imewarejesha katika nchi zao makumi ya maelfu ya wahajiri wa Kiafrika waliokuwa wamemiminika katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Hayo yalisemwa jana na Nouredine Bedoui, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Algeria na kufafanua kuwa, tokea mwaka 2015 hadi sasa, nchi hiyo imewarejesha nyumbani kwao wahajiri 27,000 waliokuwa nchini humo.

Amesema aghalabu ya wakimbizi hao wanatoka katika nchi za Mali, Niger, Burkina Faso na Chad na kwamba baadhi yao wamekuwa wakiingia nchini humo kinyume cha sheria kwa lengo la kutaka kwenda katika nchi za Morocco na Libya, ambazo ni vituo vikuu vya kuwasafirishia wahajiri wa Afrika kwenda barani Ulaya kusaka ajira.

Mpaka wa Algeria na Morocco

Waziri huyo wa Algeria amesisitiza kuwa, operesheni ya kuwarejesha katika nchi zao wahajiri hao wa Kiafrika itaendelea licha ya makelele ya mashirika ya kutetea haki za binadamu kama vile Human Rights Watch na Amnesty International.

Mwaka jana, Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria alitahadharisha kuwa, vijana zaidi ya elfu tano wa Afrika wamejiunga na makundi ya kigaidi katika sehemu mbali mbali duniani, hususan katika nchi za Iraq, Syria na eneo la Sahel kaskazini mwa Afrika.