Mahakama ya Juu Sierra Leone yasogeza mbele tarehe ya uchaguzi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i42258-mahakama_ya_juu_sierra_leone_yasogeza_mbele_tarehe_ya_uchaguzi
Mahakama ya Juu ya Sierra Leone imeakhirisha tarehe ya kufanyika duru ya pili ya uchaguzi wa rais hadi Machi 31.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 27, 2018 02:56 UTC
  • Mahakama ya Juu Sierra Leone yasogeza mbele tarehe ya uchaguzi

Mahakama ya Juu ya Sierra Leone imeakhirisha tarehe ya kufanyika duru ya pili ya uchaguzi wa rais hadi Machi 31.

Katika taarifa iliyotolewa jana jioni, Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini humo NEC imesema mawakili wake wamelazimika kwenda Mahakama ya Juu kuomba kusongezwa mbele tarehe ya uchaguzi huo, baada ya Mahakama Kuu ya nchi hiyo kuiagiza tume hiyo kusitisha maandalizi ya duru ya pili ya uchaguzi huo hadi pale kesi kuhusu mgogoro wa uchaguzi itakaposikizwa na kuamuliwa.

Agizo la jana limetolewa chini ya masaa 48 baada ya NEC kusisitiza kuwa duru ya pili ya uchaguzi wa rais ingefanyika leo Machi 27 kama ilivyopangwa, licha ya agizo hilo la Mahakama Kuu.

Maafisa wa NEC wakitoa taarifa kwa waandishi wa habari

Katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo uliofanyika Machi 7, mgombea wa chama cha upinzani cha SLPP, Julius Maada Bio alipata asilimia 43 ya kura dhidi ya asilimia 42 alizopata mgombea wa chama tawala cha APC, Samura Kamara.

Licha ya kuwa duru ya kwanza ilikuwa na wagombea 16, lakini kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo, wagombea wawili wa kwanza ndio wanaoruhusiwa kumenyana katika duru ya pili, iwapo hakuna muwaniaji atakayepata kwa uchache asilimia 55 ya kura zote halali zilizopigwa katika duru ya kwanza.