Kikosi cha MONUSCO chaongezewa muda wa kuhudumu DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i42304-kikosi_cha_monusco_chaongezewa_muda_wa_kuhudumu_drc
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekiongezea muda wa kuhudumu kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo MONUSCO.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 28, 2018 02:47 UTC
  • Kikosi cha MONUSCO chaongezewa muda wa kuhudumu DRC

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekiongezea muda wa kuhudumu kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo MONUSCO.

Uamuzi huo ulipasishwa jana na Baraza la Usalama kwa kauli moja ambapo mbali na MONUSCO kuongezwa muda wa mwaka mmoja mwingine kuhudumu huko Jamhuri ya KIdemokrasia ya Congo, kikosi hicho cha UN kimepewa pia jukumu la kusaidia maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao wa nchi hiyo. 

Muswada huo uliowasilishwa na Ufaransa na uliokuwa ukitaka kuongezewa muda mwingine wa mwaka mmoja kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidenmokrasia ya Congo MONUSCO ulipasishwa kwa kauli moja katika Baraza la Usalama.

Kwa mujibu wa azimio hilo, sasa kikosi cha MONUSCO kitabakia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hadi Machi mwaka 2019 ambapo mbali na majukumu yake ya kusimamia amani kinapaswa pia kusaidia mchakato na maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao wa nchi hiyo ambao unatajwa kuwa wa kihistoria.

Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

Uchaguzi mkuu ujao wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umepangwa kufanyika Disemba 23 mwaka huu na ndio unaotarajiwa kuhitimisha uongozi wa Rais Joseph Kabila ambaye amekuwa akikabiliwa na tuhuma za kufanya njama za kutaka kuendelea kubakia madarakani.

Uchaguzi wa urais katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umeahirishwa kwa zaidi ya mara mbili tangu Rais Joseph Kabila alipotakiwa kuondoka madarakani mwaka 2016 baada ya muhula wake wa uongozi kumalizika.