Wanamgambo wa kikoo kuingizwa katika Jeshi la Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i42458-wanamgambo_wa_kikoo_kuingizwa_katika_jeshi_la_somalia
Vikosi vya Umoja wa Afrika vya kulinda Amani nchini Somalia, maarufu kama AMISOM, vimetangaza kuanza kwa zoezi la kuwasajili kwa njia ya kielektroniki wapiganaji wa makundi ya wanamgambo wa kikoo katika eneo la Jubbaland, ikiwa ni mchakato wa kuwajumuisha katika jeshi la serikali katika jimbo hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 31, 2018 10:31 UTC
  • Wanamgambo wa kikoo kuingizwa katika Jeshi la Somalia

Vikosi vya Umoja wa Afrika vya kulinda Amani nchini Somalia, maarufu kama AMISOM, vimetangaza kuanza kwa zoezi la kuwasajili kwa njia ya kielektroniki wapiganaji wa makundi ya wanamgambo wa kikoo katika eneo la Jubbaland, ikiwa ni mchakato wa kuwajumuisha katika jeshi la serikali katika jimbo hilo.

Akizungumza mjini Kismayo, Mratibu wa vikosi vya AMISOM Martin Abili amesema zaidi ya wanajeshi 5000 wa vikundi hivyo watasajiliwa katika miji ya Gedo, Juba Kusini na Jubba ya Kati.

Amesema usajili huo wa kielektroniki unalenga kukusanya taarifa binafsi za msingi ikiwemo picha, na alama za vidole za kila mwanajeshi.

Abili amefafanua kwamba wanajeshi hao watajumuishwa katika kikosi cha polisi wa mjini Jubbaland, au askari wa jimbo au Jeshi la Kitaifa  la Somalia.

Askari wa Kulinda amani wa Umoja wa Afrika nchini Somalia

Naye Kamanda wa Jeshi la Jubbaland Brigedia Jenerali Adam Mohamud Ibrahim amesema zoezi hilo ni muhimu katika eneo hilo na kwamba wako tayari kusaidia ili usajili huo ukamilike.

Kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM kinaundwa na jumla ya askari 22,000 kutoka Kenya, Uganda, Burundi na Ethiopia na kipo katika nchi hiyo kwa ajili ya kupambana na kundi la wanamgambo wa al-Shabab.