Rais wa Somalia asimamisha kikao cha kumuuzulu Spika wa Bunge
Rais Mohammed Abdullahi Farmajo wa Somalia jana alilazimika kusimamisha kikao cha Bunge la Federali la nchi hiyo kilichokusudia kumuengua madarakani Spika wa bunge hilo.
Hoja ya kutaka kumuzuklu Spika wa Bunge hilo sasa haitajadiliwa tena kwa kuwa muda wake wa kisheria umepita, na sasa mgogoro huo unatazamiwa kupatiwa ufumbuzi kwa njia ya mazungumzo.
Juzi usiku Rais Farmajo aliwaweka kwenye kiti moto Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Hassan Ali Khaire, Spika wa Bunge Mohamed Osman Jawari na manaibu wake wawili, kujadili mzozo huo.
Somalia imeshuhudia malumbano makali baina ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo pamoja na kundi la wabunge wanaomuunga mkono kwa upande mmoja na na Spika wa Bunge la nchi hiyo ya Pembe ya Afrika kwa upande mwingine.
Mgogoro huo ulianza mapema mwezi jana, baada ya wabunge zaidi ya 100 wanaoegemea upande wa Waziri Mkuu, kuwasilisha hoja bungeni ya kutaka kuenguliwa madarakani Spika wa bunge, kwa madai kuwa amekuwa kizingiti kwenye shughuli za bunge hilo.
Jumatatu iliyopita, Jumuiya ya Maendeleo ya Kiserikali ya Nchi za Afrika Mashariki IGAD ilitahadharisha kuwa, mkwaruzano huo unaoshuhudiwa hivi sasa miongoni mwa viongozi wa ngazi za juu wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika huenda ukasababisha kuporomoka kwa mafanikio yaliyopatikana kwa ajili ya kuinasua nchi hiyo kutoka kwenye kinamasi cha ukosefu wa usalama na uthabiti.