Ripoti: Kinara wa upinzani Congo alichukua uraia wa Italia
Ripoti kutoka Italia zimefichua kuwa, kinara wa kambi ya upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Moise Katumbi alichukua uraia wa Italia kuanzia mwaka 2000 hadi 2017.
Ripoti hiyo iliyofichuliwa na maafisa wa mji alikokua akiishi wa San Vito dei Normanni inaweka mashakani matumaini ya Moise Katumbi ya kugombea urais kama kinara wa upinzani katika uchaguzi mkuu unaotazamiwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo alisema wiki iliyopita kwamba, ameanzisha uchunguzi kuhusu madai kwamba, Katumbi ni raia wa Italia baada ya habari hiyo kuripotiwa kwanza na jarida la Jeune Afrique lenye makao yake Paris nchini Ufaransa.
Kwa mujibu wa katiba ya Congo DR, wananchi wa nchi hiyo hawaruhusiwi kuwa na uraia wa nchi mbili na wanapaswa kuomba tena uraia iwapo itabainika kuwa walichukua uraia wa nchi nyingine.

Mji wa San Vito dei Normanni ulioko kusini mwa Italia umethibitisha kuwa, Moise Katumbi alichukua uraia wa Italia kwa zaidi ya miaka 16.
Katumbi mwenyewe amesema hakuna mtu anayeweza kumnyang'anya uraia wake wa Congo ingawa hajakanusha kwamba alichukua uraia wa Italia.
Milionea huyo anatazamwa kama kinara wa kambi ya upinzani katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Disemba mwaka huu.