AMISOM: Hatutahusika kwa namna yoyote katika mgogoro wa kisiasa nchini Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i42768-amisom_hatutahusika_kwa_namna_yoyote_katika_mgogoro_wa_kisiasa_nchini_somalia
Kikosi cha Askari wa Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika AU nchini Somalia AMISOM kimetoa taarifa kikikanusha kuhusika kwa namna yoyote katika mkwamo wa kisiasa wa hivi sasa ndani ya serikali ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 07, 2018 11:43 UTC
  • AMISOM: Hatutahusika kwa namna yoyote katika mgogoro wa kisiasa nchini Somalia

Kikosi cha Askari wa Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika AU nchini Somalia AMISOM kimetoa taarifa kikikanusha kuhusika kwa namna yoyote katika mkwamo wa kisiasa wa hivi sasa ndani ya serikali ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Francisco Madeira, mjumbe maalumu wa AU nchini Somalia sambamba na kusisitizia udharura wa kuheshimiwa haki ya kujitawala taifa la Somalia, amesema kuwa AMISOM hairuhusiwi kuzingira bunge hadi pale itakapopewa amri na serikali kuu ya Mogadishu. Madeira ameongeza kuwa, ombi lililotolewa na baadhi ya viongozi wa nchi hiyo la kutaka kudhibitiwa usalama wa bunge, linaweza kutekelezwa kupitia kuheshimiwa kikamilifu sheria za nchi hiyo.

Bunge la Somalia

Matamshi hayo ya kiongozi huyo wa Umoja wa Afrika yametolewa baada ya Paul Lokech, kamanda wa Kikosi cha Askari wa Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM kutangaza kuwa askari wa kikosi hicho waliamua kusimamia usalama wa bunge Jumatano iliyopita baada ya kushuhudiwa mkwamo wa kisiasa nchini humo. Baadhi ya duru za habari nchini humo zimeripoti kwamba, serikali ya Mogadishu haikufurahishwa na uingiliaji wa askari hao wa AMISOM katika kikao cha wabunge cha siku ya Jumatano kilichofanyika kwa lengo la kupiga kura ya kutokuwa na imani na Spika wa Bunge.

Mohamed Osman Jawari, Spika wa Bunge la Somalia

Mohamed Osman Jawari, Spika wa Bunge la Somalia anatuhumiwa na wabunge kuwa anatumia vibaya madaraka yake na kuzuia kufanyiwa marekebisho katiba ya nchi hiyo. Ni muda sasa mgogoro wa kisiasa nchini Somalia umeendelea kushika kasi tangu Rais Mohamed Abdullahi Mohamed alipochukua hatua za kuwapiga kalamu nyekundu viongozi wa ngazi ya juu serikalini.