Watu 18 wauawa katika hujuma dhidi ya kanisa nchini Nigeria
Kundi la watu waliobeba silaha limeshambulia kanisa moja la Kikatoliki nchini Nigeria na kuua watu wasiopungua 18.
Moses Yamu, Msemaji wa Polisi katika jimbo la Benue amesema shambulizi hilo la kikatili lilitokea alfajiri ya jana Jumanne katika kijiji cha Ayar Mbalom, eneo la Gwer Mashariki ambapo watu wengine kadhaa walijeruhiwa pia.
Amesema watenda jinai hao wanaoaminika kuwa wafugaji wa kabila la Fulani walilivamia kanisa la Katoliki la St. Ignatius huku wakiwa wamejizatiti kwa bunduki na kuwamiminia risasi watu waliokuwa kwenye kanisa hilo, na kuua 16 miongoni mwao wakiwemo mapadri wawili.
Hujuma hii inajiri chini ya wiki moja baada ya mashambulizi pacha ya mabomu kuua waumini watatu wa Kiislamu huku wengine tisa wakijeruhiwa wakiwa ndani ya msikiti katika mji wa Bama jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Aidha mapema mwaka huu, gaidi wa kundi la kitakfiri la Boko Haram aliyejifunga bomu mwilini alijiripua na kuua watu wasiopungua 14 ndani ya msikiti mmoja katika mji wa Gamboru ulioko kwenye jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Kundi hilo lililoanzisha uasi mwaka 2009 kwa madai ya kupinga elimu zinazotoka Magharibi huwa kwa kawaida linawatumia watu wanaojiripua wakiwemo wanawake na wasichana kufanya mashambulio ya aina hiyo, katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu kama misikitini, makanisani na masokoni.