Rais wa Sudan Kusini apinga wito wa wapinzani wa kujiuzulu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i43628-rais_wa_sudan_kusini_apinga_wito_wa_wapinzani_wa_kujiuzulu
Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini amepinga wito uliotolewa na wapinzani nchini humo waliomtaka ajiuzulu kama sehemu ya jitihada za kuhitimisha vita vya ndani. Rais Kiir ameyatuhumu makundi yanayopinga serikali yake kwa kuwasilisha matakwa yasiyo ya kimantiki katika mazungumzo ya amani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 25, 2018 09:27 UTC
  • Rais wa Sudan Kusini apinga wito wa wapinzani wa kujiuzulu

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini amepinga wito uliotolewa na wapinzani nchini humo waliomtaka ajiuzulu kama sehemu ya jitihada za kuhitimisha vita vya ndani. Rais Kiir ameyatuhumu makundi yanayopinga serikali yake kwa kuwasilisha matakwa yasiyo ya kimantiki katika mazungumzo ya amani.

Mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliikumba Sudan Kusini miaka miwili baada ya nchi hiyo kujipata uhuru na kuuwa makumi ya maelfu ya watu. Katika mazungumzo yaliyofanyika mwezi uliopita huko Addis Ababa mji mkuu wa Ethiopia chini ya uenyekiti wa Jumuiya ya Igad, makundi kumi ya upinzani ya Sudan Kusini yalimtaka Rais Salva Kiir wa nchi hiyo ajiuzulu kiti cha urais.

Makundi hayo pia yalitaka kuvunjwa bunge la mpito na kuundwa jingine jipya litalokuwa na wabunge chini ya 200.  Akizungumza katika shughuli za mazishi za aliyekuwa mkuu wa majeshi wa Sudan Kusini Jenerali James Ajonga, Rais Kiir amesema kuwa, watu wanaopigana dhidi ya serikali yake wana masharti yasiyo ya kimantiki kwa ajili ya kusaka amani.

Mwendazake Jenerali James Ajonga, mkuu wa zamani wa majeshi wa Sudan Kusini 

Inafaa kukumbusha hapa kuwa makundi ya waasi na serikali ya Sudan Kusini mwezi Disemba mwaka jana yalisaini makubaliano ya kusitisha vita huko Addis Ababa Ethiopia hata hivyo makubaliano hayo yalikiukwa masaa machache baada ya kusainiwa.