Watu 11 wauawa Nigeria, misikiti 2 yachomwa moto
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i43674-watu_11_wauawa_nigeria_misikiti_2_yachomwa_moto
Kwa akali watu 11 wameuawa katika jimbo la Benue, katikati mwa Nigeria katika mapigano ya kikabila, siku moja baada ya watu wengine 18 kuuawa wakiwa kanisani katika jimbo hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 26, 2018 10:54 UTC
  • Watu 11 wauawa Nigeria, misikiti 2 yachomwa moto

Kwa akali watu 11 wameuawa katika jimbo la Benue, katikati mwa Nigeria katika mapigano ya kikabila, siku moja baada ya watu wengine 18 kuuawa wakiwa kanisani katika jimbo hilo.

Rilwanu Adamu, mshauri wa Gavana Samuel Ortom wa jimbo hilo katika masuala ya dini amesema mauaji hayo yalifanyika jana Jumatano katika mji wa Makurdi, makao makuu ya jimbo la Benue.

Amesema waliofanya mauaji hayo waliwalenga wafanyabiashara wa kabila la Kihausa na kwamba watu wengine watano wamejeruhiwa na kulazwa katika hospitali moja mjini Makurdi.

Rilwanu Adamu, mshauri wa Gavana Samuel Ortom wa jimbo la Benue ameongeza kuwa, misikiti miwili imeteketezwa kwa moto na kubakia majivu sawa na bidhaa za wafanyabiashara Waislamu wa kabila la Hausa katika mji huo.

Moja ya misikiti iliyochomwa moto na kuvunjwa na maadui wa Uislamu nchini Nigeria

 

Jumanne iliyopita, kundi la watu waliobeba silaha lilishambulia kanisa moja la Kikatoliki nchini Nigeria na kuua watu wasiopungua 18 katika kijiji cha Ayar Mbalom, eneo la Gwer jimboni Benue, wiki moja baada ya mashambulizi pacha ya mabomu kuua waumini watatu wa Kiislamu huku wengine tisa wakijeruhiwa wakiwa ndani ya msikiti katika mji wa Bama jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Kutokana na kushtadi mauaji hayo ya kikabila na kidini nchini Nigeria, Bunge la nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika jana lilipiga kura ya kumtaka Rais Muhammadu Buhari wa nchi hiyo afike mbele yake kutoa maelezo juu ya kuongezeka mashambulizi hayo, huku likitaka maafisa wote wakuu wa usalama wapigwe kalamu nyekundu.