Mshambuliaji wa kujitoa mhanga aua maafisa wanne wa jeshi la Somalia
Mshambuliaji wa kujitoa mhanga ameua maafisa wanne wa jeshi la Somalia baada ya kujiripua katika kambi moja ya jeshi iliyoko kwenye mji wa Galkayo. Maafisa wa jeshi wamesema kundi la kigaidi la Ash-Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda ndilo lililohusika na shambulio hilo.
Meya wa mji wa Galkayo Hirsi Yusuf Barre amesema, kamanda mmoja na makanali wawili wa jeshi ni miongoni mwa maafisa waliouawa katika shambulio hilo la leo.
Kambi hiyo ya jeshi ni makao ya kikosi cha wanajeshi kutoka maeneo mawili ya Somalia yenye mamlaka yao ya ndani ya Puntland na Galmudug ambao wamejumuishwa kwenye jeshi la serikali ya shirikisho ya Somalia ikiwa ni katika jitihada za kuiunganisha nchi hiyo iliyokumbwa na mpasuko.
Afisa wa polisi ya Somalia Abdirahman Haji amesema idadi ya vifo inaweza kuongezeka.
Msemaji wa operesheni za kijeshi za kundi la kigaidi la Ash-Shabaab Abdiasis Abu Musab amesema, kundi hilo limeua watu watano katika shambulio hilo.
Kundi la kigaidi na ukufurishaji la Ash-Shabaab limekuwa likifanya hujuma na mashambulio kwa lengo la kuiangusha serikali kuu ya Somalia ili kuasisi utawala unaotokana na ufahamu potofu na fikra mgando kuhusu sharia za Kiislamu.
Tangu mwaka 2011 lilipofurushwa katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, kundi la Ash-Shabaab limepoteza udhibiti wa karibu miji yote mikubwa na midogo liliyokuwa likiishikilia, lakini lingali linaendelea kufanya hujuma na mashambulio ya kigaidi katika maeneo mengine nje ya Mogadishu.../