UN yaonya kuhusu hatari ya kuongezeka machafuko Sudan Kusini
Mkuu wa timu ya Umoja wa Mataifa ya kusimamia amani Sudan Kusini ametahadharisha kuhusu kuongezeka machafuko katika kipindi hiki cha kukaribia mazungumzo ya amani nchini humo.
David Shearer amesema hayo na kuongeza kuwa, vyama na mirengo yote ya Sudan Kusini ina wajibu wa kukomesha mapigano na kurejesha utulivu na amani nchini humo.
Mkuu huyo wa timu ya Umoja wa Mataifa ya kusimamia amani Sudan Kusini aidha amesema, makundi ya umoja huo yaliyotumwa katika kona mbalimbali za nchi hiyo yamekuwa yakiripoti kutokea jinai na uhalifu wa kila namna kama vile mauaji, mashambulizi, machafuko, udhalilishaji wa kijinsia, kuchomwa moto nyumba, kuvamiwa mifugo pamoja na kushambuliwa shule na mahospitali.
Wimbi jipya la machafuko ya Sudan Kusini katika kipindi hiki cha kukaribia mazungumzo ya amani ya mwezi ujao wa Mei 2018, limeyatia hatarini maisha ya maelfu ya watu wa maeneo tofauti ya nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.
Ripoti zinasema kuwa, zaidi ya wafanyakazi 30 wa kutoa misaada ya kibinadamu wamehamishiwa katika maeneo yaliyo salama zaidi katika kipindi cha wiki mbili zilizopita na maelfu ya wananchi wa nchi hiyo wamekimbia maeneo yenye machafuko na kukimbilia misituni na milimani.
Duru nyingine ya mazungumzo ya amani ya Sudan Kusini inatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 17 hadi 21 mwezi ujao wa Mei baada ya kusimama wiki zilizopita kutokana na ugomvi na mizozo baina ya pande hasimu.