Amisom, Jeshi la Somalia waimarisha usalama kuelekea Ramadhani
Kikosi cha Kusimamia Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (Amisom) kimetangaza mkakati mpya wa kutibua shambulizi lolote tarajiwa la kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab, ikiwa imesalia chini ya wiki mbili kuanza mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Brigedia Paul L'Okech, kamanda wa askari wa Uganda wanaohudumu chini ya Amisom amewaambia waandishi wa habari kuwa, sehemu kubwa ya mkakati huo wa kiusalama itatekelezwa na Jeshi la Taifa la Somalia SNA na Jeshi la Polisi la nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Amefafanua kuwa, "Kimsingi genge la al-Shabaab hushadidisha hujuma zake katika mwezi Ramadhani na haswa katika mji mkuu Mogadishu na viunga vyake, lakini Amisom na vikosi vya usalama vya Somalia vimechukua hatua za tahadhari za kuzuia shambulizi lolote katika mwezi huo."
Kundi la kigaidi na ukufurishaji la al-Shabaab limekuwa likifanya hujuma na mashambulio kwa lengo la kuiangusha serikali kuu ya Somalia ili kuasisi utawala unaotokana na ufahamu potofu na fikra mgando kuhusu sharia za Kiislamu.
Tangu mwaka 2011 lilipofurushwa katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, kundi la Ash-Shabaab limepoteza udhibiti wa karibu miji yote mikubwa na midogo liliyokuwa likiishikilia, lakini lingali linaendelea kufanya hujuma na mashambulio ya kigaidi katika maeneo mengine nje ya Mogadishu.
Kundi hilo lilianzisha hujuma zake nchini Somalia mwaka 2007 kwa lengo la kuiondoa madarakani serikali ya nchi hiyo linayoituhumu kuwa ni serikali ya kikafiri.