AMISOM kupeleka maafisa wa polisi katikati mwa Somalia
Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM kimetangaza mpango wake wa kutuma maofisa wa polisi kwenye eneo la Hirran, katikati kusini mwa Somalia.
AMISOM inasema ujumbe wake unaoongozwa na mratibu wa operesheni ya polisi ya AMISOM Bw. Daniel Ali Gwambal umefanya ziara Beletweyne wiki iliyopita kukagua maandalizi ya kutuma polisi huko Hirran.
Ujumbe wa AMISOM pia umekagua vifaa vitakavyotumiwa na kundi hilo lenye polisi 32 kutoka Nigeria.
Haruna Ismail, Kamanda wa Kikosi cha Polisi ya Nigeria katika Amisom amesema, mipango imekamilika na kwamba timu yake itafika eneo hilo kuimarisha usalama. Amesema maafisa hao wa Nigeria pia watahusika katika kuwapa mafunzo Polisi ya Somalia katika eneo hilo la Beletwenyne.

Wakati huohuo Kamanda wa AMISOM ameonya kuhusu mpango wa kupunguza askari wa kulinda amani Somalia. Brigedia Jenerali Paul Lokech wa Uganda amesema kupunguzwa askari wa AMISOM kutakuwa na athari mbaya katika nchi hiyo. Magaidi wa al Shabab wangali ni tishio katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Umoja wa Mataifa ambao unafadhili askari hao wa AMISOM umetaka kuanzishwa operesheni ya kupunguza askari hao ambao sasa ni 21,000. Wanajeshi wa AMISOM walioko Somalia ni kutoka Uganda, Kenya, Burundi, Somalia, Ethiopia, Djibouti na Sierra Leone. Nao maafisa wa polisi wa AMISOM ni kutoka Nigeria, Sierra Leone na Uganda.