May 12, 2018 07:35 UTC
  • Iran yalaani shambulizi dhidi ya Waislamu msikitini Afrika Kusini

Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali shambulizi la hivi karibuni dhidi ya msikiti mmoja karibu na mji wa Durban nchini Afrika Kusini.

Katika taarifa, Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani shambulizi hilo, ambalo anasisitiza kuwa limetekelezwa kwa lengo la kuzusha taharuki, kuvuruga usalama na kuchochea mifarakano ya kimadhehebu.

Kadhalika ametoa mwito wa kuanzishwa uchuguzi mara moja wa tukio hilo na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria wahusika wa hujuma hiyo ya juzi Alkhamisi.

Aidha Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amezitaka nchi zote kuwa macho na kuunga mkono kwa dhati vita dhidi ya ugaidi na makundi ya kitakfiri yenye misimamo ya kufurutu ada.

Msikiti wa Imam Hussein AS nchini Afrika Kusini

Alkhamisi iliyopita nyakati za Alasiri, magaidi waliokuwa na silaha waliuvamia Msikiti wa Imam Hussein AS wa Waislamu wa madhehebu ya Shia katika mji mdogo wa Verulam nje ya Durban na kuwashambulia kwa visu waumini walikuwemo hapo akiwemo Imamu wa msikiti huo.

Imamu huyo aliuawa shahidi kwa kukatwa kichwa na magaidi huo, huku waumini wengine waliodungwa visu wakijeruhiwa vibaya.

Jumuiya ya Maulamaa Afrika Kusini imetoa taarifa na kulaani mauaji hayo na kusema yanalenga kuibua taharuki, na hali ya kutokuaminiana katika jamii, huku Idara ya Polisi ikisema haiwezi kustahamili jinai kama hiyo na kwamba maafisa wa usalama wanachunguza tukio hilo. 

Tags