Muda wa kuhudumu kikosi cha AU cha kulinda amani Somalia waongezwa
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepasisha kwa kauli moja suala la kurefushwa kazi za kikosi cha Umoja wa Afrika AU cha kulinda amani nchini Somalia kinachojulikana kwa jina la AMISOM.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mtaifa limerefusha muda wa kazi za kikosi hicho nchini Somalia hadi tarehe 31 Julai mwaka huu.
Somalia ni moja ya nchi maskini zaidi na yenye ukosefu mkubwa zaidi wa utulivu na amani duniani na kwa miaka kadhaa sasa serikali ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika inasaidiwa na kikosi cha Umoja wa Afrika AMISOM kupambana na magaidi wa al Shabab.
Kikosi cha AMISOM huko Somalia kinaundwa na wanajeshi 21,600 kutoka nchi mbalimbali za Afrika na kinafanya kazi zake kwa baraza kamili za Umoja wa Mataifa na kwa msaada wa kifedha wa umoja huo.
Sambamba na kurefusha muda wa kikosi hicho hadi mwisho mwa mwezi Julai, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeruhusu pia kupitiwa mapendekezo yanayotarajiwa kuwemo katika ripoti ya pamoja ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa kuhusu Somalia. Ripoti hiyo inatarajiwa kutolewa tarehe 15 mwezi ujao wa Juni.
Kazi za kikosi cha AMISOM zilianza mwaka 2007 huko Somalia kwa ajili ya kuisaidia serikali dhaifu iliyokuwa inaungwa mkono kimataifa, kupambana na genge la kigaidi la al Shabab.
Jeshi la Somalia lina mapungufu mengi yakiwemo ya uchache wa zana na kutokuwa na usimamiaji mzuri hivyo linaliwia vigumu kupambana na magaidi wa al Shabab ila kwa msaada wa kimataifa.