Makamanda saba wa Al Shabab wauawa Somalia
Makamanda saba wa kundi la kigaidi la Al Shabab wameuawa Somalia katika oparesheni za pamoja za Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika Somalia AMISOM na jeshi la nchi hiyo.
Taarifa zinasema makamanda hao wa ngazi za juu wa magaidi wakufurishaji wa Al Shabab wameuawa katika kipindi cha wiki moja kufuatia oparesheni za askari wa AMISOM na Jeshi la Somalia. Tarehe Pili mwezi huu kamanda wa Al Shabab huko Janaale Abdirashid Bugdube, aliuawa. Aidha makamanda wengine wa Al Shabab walioangamizwa katika oparesheni hizo za pamoja ni Aden Bale – kamanda wa Al-Shabab eneo la Leego ; Sheikh Mohamed Ali aliyekuwa naibu kamanda eneo la Janaale, Mohamed Abribao aliyekuwa jaji wa Al-Shabaab huko huko Janaale, Hassan Ali Dole, mkuu wa shirika la kijasusi la Al Shabab (Amniyat) eneo la Lower Shabbele, raia wa Yemen aliyekuwa mtaalamu wa mabomu ya kutegwa kando ya barabara IED aliyejitambulisha kama Abu Islam na raia wa Kenya Sheikh Mansur ambaye alikuwa kiongozi wa kutoa mafunzo kwa magaidi wa Al Shabab. Akitoa taarifa hiyo kamanda mwandamizi wa AMISOM Brigedia Jenerali Sam Okiding amesema magaidi wa Al Shabab wamepata pigo kubwa na sasa wanaogopa kukabiliana ana kwa ana na askari wa AMISOM.
Jeshi la Somalia linapambana na magaidi wa al-Shabab kwa kushirikiana na Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM chenye askari 22,000 katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.