ICC: Naibu Rais wa Kenya hana kesi ya kujibu
Mahakama ya Kimatiafa ya Jinai ICC imetangaza kuwa Naibu wa Rais wa Kenya William Ruto na mwanahabari Joshua Sang hawana kesi ya kujibu kufuatia kuvurugika mkondo wa kesi dhidi yao.
Majaji wamepitisha kwa wingi wa kura uamuzi wa kutupilia mbali kesi hiyo kwa msingi kuwa mashahidi wamekuwa wakikana ushahidi waliotoa huku kukiwa na uingiliaji wa kisiasa katika kesi hiyo.
Katika uamuzi uliotiwa saini na Jaji Eboe Usuji, majaji wa ICC hata hivyo wamesema uamuzi wao haumaanishi kuwa wawili hao hawawezi kushtakiwa siku za usoni ICC au katika mahakama ya kitaifa Kenya. Jaji Robert Fremr amesema washukiwa hawana kesi ya kujibu kwa kuzingatia kuwa ushahidi wa upande wa mashtaka ulikiuka taratibu za mahakama. Hata hivyo Jaji wa tatu katika kesi hiyo Bi. Hererra Carbuccia alipinga uamuzi wa majaji wenzake wawili. Ruto na Sang walikuwa wanakabiliwa na mashtaka ya jinai dhidi ya binadamu katika ghasia za baada uchaguzi wa mwaka 2007/2008 nchini Kenya ambapo watu 1,113 walipoteza maisha na wengine zaidi ya nusu milioni kuachwa bila makao.
Mahakama ya ICC imesema waathirika wanaweza kuwasilisha pingamizi zao kuhusu uamuzi wa leo.
Mawakili Karim Khan wa Ruto na Katwa Kigen wa Sang wamesema kesi hiyo imesambaratika kutokana na upande wa mashtaka kutokuwa na ushahidi. Mwezi Machi mwaka 2015 ICC pia ilitupilia mbali kesi kama hivyo dhidi ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta. Kabla ya hapo mahakama hiyo pia ilifuta kesi kama hiyo ya mwanasiasa maarufu wa Kenya Henry Kosgei Septemba 2011 huku kesi dhidi ya aliyekuwa kamishna wa polisi Kenya Hussein Ali ikitupiliwa mbali Januari 2012. Kufuatia uamuzi wa leo, kesi zote za Wakenya sita ICC zimetupiliwa mbali na mahakama hiyo yenye makao yake The Hague.