Shambulio la bomu Benghazi, Libya laua watu saba
Kwa akali watu saba wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya gari lililokuwa limesheheni mabomu kuripuka katika barabara yenye shughuli nyingi mjini Benghazi, mashariki mwa Libya.
Duru za habari zinaarifu kuwa, hujuma hiyo imetokea mapema leo karibu na Hoteli ya Tibesti, ambayo inahesbiwa kuwa mgahawa mkubwa zaidi katika mji huo wa kistratajia ambao unadhibitiwa na vikosi vya Jenerali Khalifa Haftar.
Miongoni mwa waliouawa ni mtoto mdogo wa kike, huku habari zaidi zikisema watu wasiopungua kumi wamejeruhiwa.
Februari mwaka huu watu karibu 50 walipoteza maisha na kujeruhiwa katika mji huo wa Benghazi kufuatia hujuma ya kigadi msikitini wakati wa Sala ya Ijumaa, wiki chache baada ya watu wengine wasiopungua 33 kuuawa baada ya magari mawili yaliyotegwa mabomu kuripuka katika mji huo ulioko mashariki mwa Libya.
Mji huo ambao ulikuwa kituo kikuu cha mapinduzi ya mwaka 2011 na makao makuu ya wanamapinduzi waliomuondoa madarakani Kanali Muammar Gaddafi, umekuwa katika ghasia na machafuko yaliyoanza Mei mwaka 2014 hadi sasa.