Wasiwasi wa AU kuhusu madola yasiyo ya Afrika kuingilia mambo ya Somalia
Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Bw. Moussa Faki Mahamat ameeleza wasiwasi kuhusu ongezeko la uingiliaji wa nje unaofanywa na madola yasiyo ya Afrika katika mambo ya ndani ya Somalia.
Bw. Faki amesema hayo alipokutana na Waziri Mkuu wa Somalia Bw. Ali Khaire nchini Ethiopia, na kuongeza kuwa hatua hizo zinatishia kuharibu juhudi za ujenzi wa amani na taifa zinazoendelea nchini Somalia.
Amesema uingiliaji huo unahatarisha maendeleo yaliyopatikana kupitia juhudi za pamoja za tume ya AMISOM na jeshi la Somalia. Amezitaka pande za nje kuepuka kuchukua hatua zinazoweza kuharibu mchakato wa maendeleo ya Somalia.
Kauli hiyo ya Mkuu wa Tume ya AU inakuja baada ya Serikali ya Kenya kuzitahadahrisha nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi, hasa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kuacha kuchochea mgogoro wa Somalia na kuidhoofisha serikali ya nchi hiyo.
Kenya imetangaza uungaji mkono wake kwa serikali ya Rais Mohamed Abdullahi 'Farmajo' wa Somalia na kuzikosoa kwa njia isiyo ya moja kwa moja nchi ambazo zina mikataba ya kibiashara na kijeshi na maeneo ya Somaliland na Puntland. Serikali ya Kenya inasema mikataba kama hiyo inaweza kuidhoofisha serikali ya Somalia.
Katika hotuba yake ya kila mwaka bungeni hivi karibuni, Rais Uhuru Kenyatta aliashiria kwa njia ya moja kwa moja kuwa baadhi ya madola ya kigeni yanavuruga msingi wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika Somalia Amisom. Alisema lengo la uingiliaji huo ni kuidhoofisha serikali kuu ya Somalia.
Serikali ya Somalia imekataa kujiunga na Saudi Arabia, UAE, Bahrain na Misri katika kuitenga Qatar kwenye mgogoro unaotokota wa Ghuba ya Uajemi. Hatua hiyo ya serikali ya Mogadishu inaonekana kuzikasirisha tawala hizo ambazo sasa zinalenga kuidhoofisha serikali hiyo.
Serikali ya Somalia imewasilisha malalamiko ya kimatiafa dhidi ya UAE baada ya nchi hiyo kutia saini mkataba wa kijeshi na kibiashara na eneo lilolojitangazia uhuru la Somaliland.