Mahasimu wa kisiasa nchini Libya waafikiana kuhusu tarehe ya uchaguzi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i45138
Pande hasimu za kisiasa nchini Libya zimeafikiana kuhusu kufanyika uchaguzi wa rais na wa bunge nchini humo Disemba 10 mwaka huu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 29, 2018 14:02 UTC
  • Mahasimu wa kisiasa nchini Libya waafikiana kuhusu tarehe ya uchaguzi

Pande hasimu za kisiasa nchini Libya zimeafikiana kuhusu kufanyika uchaguzi wa rais na wa bunge nchini humo Disemba 10 mwaka huu.

Taher al-Sonni, Mshauri wa Waziri Mkuu wa Libya, Fayez Faraj amesema kuwa, tarehe hiyo ya uchaguzi imeafikiwa baada ya pande hasimu nchini humo kukutana hii leo mjini Paris, Ufaransa kwa madhumuni ya kufikia makubaliano juu ya ramani ya njia ya kisiasa inayolenga kutatua masuala yanayozozaniwa na pande hizo, ili kuandaa mazingira ya kufanyika uchaguzi.

Ameongeza kuwa, pande nne za kisiasa zilizoshiriki mkutano huo aidha zimekubaliana kuhusu kutamatisha mchakato wa katiba ambayo itakuwa msingi wa uchaguzi huo, kufikia Septemba 16.  

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya Ghassan Salame anaendeleza juhudi zinazolenga kuiunganisha tena Libya na kurejesha uthabiti nchini humo baada ya kupita miaka saba tangu lililipotokea vuguvugu la umma lililouangusha utawala wa Muammar Gaddafi na hatimaye kupelekea kuuawa kiongozi huyo aliyeitawala Libya kwa miongo kadhaa.

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Ghassan Salame na Fayez Siraj

Miongoni mwa shakhsia walioshiriki mkutano wa leo mjini Paris ni Waziri Mkuu wa Libya Fayez al-Sarraj, kamanda wa mashariki mwa Libya Jenerali Khalifa Haftar, Spika wa Baraza la Wawakilishi la eneo hilo Aguila Saleh pamoja na Khaled Al-Mishri, rais wa Baraza Kuu la Dola.

Joseph Muscat, Waziri Mkuu wa Malta amesema baada ya mkutano huo kuwa, "Muelekeo chanya! Pande zote husika katika mkutano wa Paris zimekubaliana kuhusu kufanyika uchaguzi kufikia Disemba, tuwe na matumaini kwamba pande hizo zitalipa umuhimu suala hilo, na pia sisi tuna jukumu la kuwasaidia katika kufanikisha mchakato huo."