Ethiopia yakubali makubaliano ya amani na hasimu wa muda mrefu, Eritrea
Ethiopia imetangaza kuwa itakubali masharti ya makubaliano ya amani na Eritrea ya mwaka 2000, katika hatua inayonuia kupunguza taharuki na msuguano wa miongo kadhaa na jirani yake huyo.
Serikali ya Addis Ababa imetoa tangazo hilo masaa machache baada ya kufuta sheria ya hali ya hatari, ikiwa ni katika mfululizo wa mageuzi yanayofanywa na Waziri Mkuu mpya, Abiy Ahmed.
Fitsum Arega, Afisa Mkuu katika Afisi ya Waziri Mkuu amesema, "Serikali ya Eritrea pia inapaswa kuchukua hatua kama yetu ya kukubali makubaliano ya amani ya mwaka 2000 ambayo yalihitimisha vita vya miaka miwili kati ya nchi mbili hizi. Pande zote mbili zimepata hasara isiyoelezeka kutokana na kugonga mwamba mchakato wa amani. Hali hii inafaa kubadilika kwa maslahi ya pande zote husika."
Mwezi Machi mwaka huu, Ethiopia iliituhumu jirani yake Eritrea kuwa ilichangia kuvuruga usalama wake kwa kuyaunga mkono 'makundi haribifu' katika kipindi ambapo sheria ya hali ya hatari ilikuwa inatekelezwa nchini humo. Ethiopia ilitangaza sheria ya hali ya hatari tarehe 18 ya mwezi wa Februari kufuatia kujiuzulu waziri mkuu wa nchi hiyo Hailemariam Desalegn.
Itakumbukwa kuwa Ethiopia na jirani yake Eritrea ziliingia vitani mara mbili kwa sababu ya mzozo wa mpaka katika kipindi cha kuanzia mwaka 1998 hadi 2000.
Eritrea, ambayo awali ilikuwa sehemu ya Ethiopia ilijitenga na nchi hiyo na kujitangazia uhuru wake rasmi mwaka 1993.