Jun 07, 2018 15:30 UTC

Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi ametangaza kuwa hatagombea urais katika uchaguzi ujao wa mwaka 2020, licha ya katiba mpya aliyoiidhinisha hii leo kumpa kibali cha kusalia madarakani hadi mwaka 2034.

Nkurunziza ambaye amekuwa madarakani tangu 2005 ametoa tangazo hilo wakati wa hafla ya kutia saini katiba mpya na kuiidhinisha rasmi iliyofanyika hii leo  katika Ikulu ya Rais mjini Gitega, katikati mwa Burundi.

Mahakama ya Katiba ya Burundi hivi karibuni ilitupilia mbali kesi iliyowasilishwa na muungano wa upinzani nchini humo kupinga matokeo ya kura ya maoni ya kuifanyia marekebisho katiba ya nchi, yaliyoipa ushindi kambi ya serikali; jambo ambalo liliuhamakisha mno upinzani nchini humo uliodai kuwa hatua hiyo ilikuwa ni njama ya Nkurunziza kuendelea kung'ang'ania madaraka.

Kwa mujibu wa matokeo rasmi ya Tume ya Uchaguzi Burundi, asilimia 73 ya wapiga kura milioni 4.3 katika zoezi hilo waliunga mkono kwa kura ya ndio kufanyika marekebisho ya katiba.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, watu wasiopungua 1,200 wameuawa katika machafuko ya Burundi tokeo Aprili mwaka 2015 hadi sasa

Licha ya tangazo hilo la kushtukiza la Nkurunziza, lakini upinzani nchini humo unashikilia kuwa, kupitishwa kwa katiba hiyo mpya kumekanyaga makubaliano ya Amani ya Arusha yaliyosainiwa mwaka 2000, ambayo yaliweka utaratibu wa kugawana madaraka miongoni mwa  makabila ya nchi hiyo. Katiba hiyo mpya imeongeza muhula wa urais kutoka miaka mitano hadi saba.

Nchi hiyo ndogo ya katikati mwa Afrika imekuwa katika mgogoro wa kisiasa tokea Aprili mwaka 2015, baada ya Nkurunziza kugombea urais kwa muhula wa tatu ambapo wapinzani walisema ni kinyume cha sheria. 

Tags