UN yaunga mkono juhudi za kuleta utulivu Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i45558-un_yaunga_mkono_juhudi_za_kuleta_utulivu_somalia
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeelezea wasiwasi wake kutokana na kuongezeka ukosefu wa usalama na hali mbaya ya kibinadamu nchini Somalia na kusisitiza kuwa inaunga mkono juhudi za kuleta utulivu katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika iliyoharibiwa vibaya na vita vya ndani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 08, 2018 00:05 UTC
  • UN yaunga mkono juhudi za kuleta utulivu Somalia

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeelezea wasiwasi wake kutokana na kuongezeka ukosefu wa usalama na hali mbaya ya kibinadamu nchini Somalia na kusisitiza kuwa inaunga mkono juhudi za kuleta utulivu katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika iliyoharibiwa vibaya na vita vya ndani.

Baraza hilo limesema katika tamko lake la baada ya kikao maalumu kilichofanyika usiku ya kuamkia leo kuhusiana na Somalia kwamba linaunga mkono hatua zilizochukuliwa na serikali ya Somalia hadi hivi sasa katika upande wa kuimarisha usalama na kufanya marekebisho ya kiuchumi na kisiasa.

Vile vile baraza hilo limeelezea wasiwasi wake kutokana mapigano ya hivi karibuni ya kaskazini mwa Somalia na kuzitaka pande zote kushirikiana na mashirika ya kimataifa na kukomesha mara moja ugomvi baina yao.

Hali ya usalama si nzuri hata kidogo nchini Somalia

Aidha wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wameelezea wasiwasi wao mkubwa kutokana na kuendelea kuweko vitendo vya kigaidi vya genge la al Shabab na kutaka juhudi za kuimarisha utawala wa sheria ziongezwe.

Katika taarifa yake hiyo baraza hilo aidha limeelezea matumaini yake kuwa kongamano la washirika wa Somalia (SPF) linalotarajiwa kufanyika tarehe 25 na 26 mwezi huu wa Juni mjini Brussels Ubelgiji litaleta manufaa ya kisiasa, kiusalama na kiuchumi kwa Somalia.