Kimbunga cha Kitropiki kimeua watu 53 Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i45886-kimbunga_cha_kitropiki_kimeua_watu_53_somalia
Shirika la Kuratibu Misaada ya Kibinadamu la Umoja wa Mataifa (OCHA) limesema watu wasiopungua 53 wamefariki dunia Somalia kufuatia kimbunga cha kitropiki kilichoikumba nchi hiyo hivi karibuni.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 15, 2018 10:45 UTC
  • Kimbunga cha Kitropiki kimeua watu 53 Somalia

Shirika la Kuratibu Misaada ya Kibinadamu la Umoja wa Mataifa (OCHA) limesema watu wasiopungua 53 wamefariki dunia Somalia kufuatia kimbunga cha kitropiki kilichoikumba nchi hiyo hivi karibuni.

Taarifa ya OCHA imesema watu  wengine takriban laki 2.29 wameathiriwa kutokana na kimbunga hicho cha kitropiki kiitwacho Sagar, ambacho kilisababisha mvua kubwa na mafuriko huko Somaliland na Puntland, kaskazini mwa Somalia mwezi uliopita.

OCHA imenukuu habari kutoka idara za usimamizi wa maafa za Somalia kuwa watu 50 wamefariki huko Somaliland na wengine watatu wamekufa katika eneo la Puntland.

Ofisa wa OCHA amesema mvua kubwa na mafuriko yameleta hasara kubwa kwa miundombinu na mashamba, na kusababisha vifo vya watu wengi na kuwafanya wengine wakose makazi. Miundombinu ya kimsingi ikiwemo maji na vifaa vya mawasiliano imeharibiwa.

Maeneo mengi katika bonde la Juba, kusini mwa Somalia pia yamekumbwa na mafuriko makubwa kutoka na mvua hizo zinazoendelea kunyesha katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Makumi ya watu wamepoteza maisha kutokana na mafuriko na maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika nchi nyingi za Afrika Mashariki.