Waziri Mkuu wa Ethiopia kutembelea eneo lenye misukosuko la kusini
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed anatarajiwa kutembelea mji wa Hawassa ambao umekuwa na vurugu zilizotokana na tofauti zilizojitokeza baina ya makabila mawili maarufu ya jimbo la kusini mwa Ethiopia.
Kwa mujibu wa Shirika la habari la Ethiopia EBC, waziri mkuu wa nchi hiyo anatarajiwa kufanya mazungumzo na wazee wa jamii hizo, pamoja na viongozi wa kiserikali wa eneo hilo ili kurejesha amani iliyotoweka.
Katika mji wa Hawassa kwa muda mrefu kumeshuhudiwa vurugu zilizopelekea vifo vingi na watu wengine kulazimika kuyahama makazi yao kutokana na tofauti za muda mrefu za haki ya umiliki na matumizi ya ardhi kati ya watu wa kabila la Sidamas ambao ni wenyeji wa eneo hilo na watu wa kabila la Wolaita. Makabila hayo mawili ni miongoni mwa makabila kadhaa ya kusini mwa Ethiopia ambayo hupigana mara kwa mara kwa sababu ya mizozo ya umiliki wa ardhi.

Mji wa Hawassa unastawi kwa kasi kiviwanda na eneo maalumu la kiviwanda ambalo lilizinduliwa Julai 2016. Ethiopia inalenga kupata pato la dola bilioni moja kwa mwaka wakati eneo hilo litakapoanza kufanya kazi kikamilifu. Kwa msingi huo serikali ya Ethiopia inajitahidi kuhakikisha kuwa amani ya kudumu inapatikana mjini Hawassa.