Mahasimu wakuu wa mgogoro wa Sudan Kusini kukutana Ethiopia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46058-mahasimu_wakuu_wa_mgogoro_wa_sudan_kusini_kukutana_ethiopia
Rais Salva Kiir wa Sudan kusini atakutana na kiongozi mkuu wa waasi, Reik Machar mjini Addis Ababa Ethiopia siku ya Jumatano kama sehemu ya jitihada za kumaliza vita vya ndani ambaرyo vimekuwa vikiendelea kwa muda wa miaka mitano nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 19, 2018 08:58 UTC
  • Mahasimu wakuu wa mgogoro wa Sudan Kusini kukutana Ethiopia

Rais Salva Kiir wa Sudan kusini atakutana na kiongozi mkuu wa waasi, Reik Machar mjini Addis Ababa Ethiopia siku ya Jumatano kama sehemu ya jitihada za kumaliza vita vya ndani ambaرyo vimekuwa vikiendelea kwa muda wa miaka mitano nchini humo.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia imetangaza kuwa, mkutano huo utafanyika chini ya usimamizi wa Waziri Mkuu Abiy Ahmed wa nchi hiyo kwa lengo la kupunguza hitilafu zilizopo baina ya Kiir na Machar.

Alhamisi pia mawaziri wa mambo ya nje wa nchini wanachama wa Jumuiya ya Kiserikali ya Maendeleo ya Mashariki Mwa Afrika IGAD watakutana katika mji huo mkuu wa Ethiopia kujadili kadhia ya Sudan Kusini na baada ya  hapo viongozi wa jumuia hiyo nao pia wanatazamiwa kukutana.

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga amekuwa akiongoza jitihada za kuwakutanisha mahasimu hao wawili na aliwahi kufika Juba na kukutana na Rais Kiir kabla ya kuelekea Afrika Kusini kukutana na Machar. Jitihada hizo za Odinga, ambaye ni mjumbe maalumu wa Kenya katika kadhia ya Sudan Kusini, zinaonekana kuzaa matunda baada ya Kiir na Machar kuafiki kukutana.

Kiongozi wa upinzani Kenya Raila Odinga akiwa na Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini

Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Nchi hiyo, ambayo ilijitenga na Sudan mwaka 2011, ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake.