Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini akutana na hasimu wake, Addis Ababa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46134-rais_salva_kiir_wa_sudan_kusini_akutana_na_hasimu_wake_addis_ababa
Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini jana alikutana na kufanya mazungumzo na kiongozi wa waasi nchini humo, Rieck Machar mjini Addis Ababa ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 2016 wakati mapatano ya amani kati ya pande hizo mbili yaliposambaratika na kuanza tena mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jun 21, 2018 03:46 UTC
  • Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini akutana na hasimu wake, Addis Ababa

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini jana alikutana na kufanya mazungumzo na kiongozi wa waasi nchini humo, Rieck Machar mjini Addis Ababa ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 2016 wakati mapatano ya amani kati ya pande hizo mbili yaliposambaratika na kuanza tena mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini.

Maafisa wa serikali ya Ethiopia wanasema mahasimu hao wawili wa kisiasa walikutana uso kwa uso baada ya kila mmoja wao kufanya mazungumzo ya faragha na mpatanishi wao, Rais Abiy Ahmed wa Ethiopia.

Mazungumzo hayo yameitishwa na serikali ya Ethiopia kwa ajili ya kukomesha mapigano ya ndani nchini Sudan Kusini ambayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwalazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.

Mazungumzo kati ya mahasimu hao wawili yamefanyika kabla ya mkutano wa leo wa jumuiya ya kikanda ya Igad. Mkutano huo unaofanyika mjini Addis Ababa utajadili suala la kurejesha amani nchini Sudan Kusini na unahudhuriwa na viongozi wa nchi wanachama.

Maamuzi ya mkutano wa leo wa Igad kuhusu Sudan Kusini yatawasilishwa katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu huko Nouakchott nchini Mauritania.